ELIMU YA MAGONJWA
Posted on: November 23rd, 2019Kujikinga na kujilinda dhidi ya magonjwa ni muhimu kwa ajili ya afya zetu. Zipo njia mbalimbali za kujikinga zidi ya magonjwa kwa njia ya maji, chakula, wanyama, wadudu na watu.
MAJI
- Vimelea wengi wanaweza “kuingia” moja kwa moja katika mwili wako kupitia maji machafu.
Namna ya kujikinga
- Njia bora zaidi ya kujikinga ni kutumia maji yaliyo safi na salama.Ukijua kwamba maji unayotumia yana vimelea au si salama, unapaswa kuyatibu. Hifadhi maji ya kunywa kwenye chombo kilichofunikwa, na uchote kwa kutumia chombo safi. Usitumbukize mikono yako kwenye chombo chenye maji safi. Inapowezekana, ishi mahali au katika nyumba zenye mfumo mzuri wa kuondoa taka ili kuepusha kuchafua vyanzo vya maji.
CHAKULA
- Vimelea hatari vinaweza kuwepo au kuingia kwenye chakula chako.
Namna ya kujikinga
- Chakula au matunda yenye bakteria, huenda yakaonekana kuwa salama na mazuri. Kwa hiyo uwe na kawaida ya kuosha vizuri matunda na mboga kabla ya kuzitumia. Hakikisha kwamba mikono yako, vyombo vya chakula, na mazingira ya jikoni, ni safi kabla ya kuanza kutayarisha na kuandaa chakula. Baadhi ya vyakula vinahitaji kupikwa kwa joto la kiwango fulani ili kuua vimelea hatari.
WADUDU
- Baadhi ya wadudu wanaweza kukuambukiza vimelea hatari vilivyo katika miili yao.
Namna ya kujikinga
- Dhibiti maambukizi yanayosababishwa na wadudu kwa kukaa ndani ya nyumba au kwa kuvaa nguo zinazofunika mwili kama vile sweta na suruali. Lala ndani ya chandarua chenye dawa, na upake dawa za kujikinga na wadudu. Ondoa vyombo vyenye maji yaliyotuama, mahali ambako mbu wanaweza kuzaliana.
WATU
- Baadhi ya vimelea vinaweza kuingia mwilini mwako kupitia umajimaji unaotoka baada ya mtu kukohoa au kupiga chafya. Pia, vimelea vinaweza kuenea kupitia kugusana kimwili kwa kukumbatiana na kusalimiana kwa mikono. Vimelea kutoka kwa watu wengine vinaweza pia kupatikana kwenye vitasa vya milango, vishikio vya ngazi, simu, rimoti, skrini za kompyuta na kibodi.
Namna ya kujikinga
- Usitumie vifaa kama vile, wembe, mswaki, au taulo na watu wengine. Epuka kugusa umajimaji kutoka kwa wanyama au watu wengine, kutia ndani damu na vitu vinavyotokana na damu. Ni muhimu sana kunawa mikono yako vizuri na kwa ukawaida. Hiyo ni moja ya njia bora za kuepuka kueneza magonjwa.