Barua Pepe | Facebook | Instagram | Twitter |

ZAIDI YA WANANCHI 700 WA MKOA WA MANYARA WAMEFANYIWA UCHUNGUZI WA MACHO

Posted on: June 13th, 2024

Wananchi waishio mkoa wa Manyara katika Kata ya Katesh –Hanang’ na Kata ya Gallapo – Babati wamejitokeza kwa wingi katika kliniki tembezi ya uchunguzi na matibabu ya macho iliyofanyika Juni 11-12, 2024.

Katika zoezi hili lilijumuisha Wataalam kutoka Hospitali ya Tumaini iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Hanang’, Wataalam wa Macho kutoka KCMC, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara na Hospitali ya Kanda Benjamini Mkapa.

Akizungumza na wananchi waliojitokeza kwaajili ya kupata huduma hii ya uchunguzi na matibabu ya macho kwa nyakati tofauti tofauti, Bi. Vailine Oswald (kwa Niaba ya Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara), amewasihi wananchi kujitokeza kupata huduma hii muhimu kwasababu Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara kwa kushirikiana na wataalam wa magonjwa ya macho wameamua kwa umoja kuwafikia wanachi walio mbalimbali na hospitali pamoja na huduma za kibingwa na kuwasogezea huduma hii.

Pia Wananchi waliofika katika kliniki hii tembezi walipongeza juhudi zinazoendelea kufanyika na  Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara kwa kuwajali wananchi waishio mkoani hapa kwa kuandaa utaratibu wa kuwafikia wananchi waishio mbalimbali na kuwapatia huduma za afya.

Wananchi waliofanyiwa uchunguzi, kati yao walipatikana na changamoto za macho na kupewa dawa na miwani na zaidi ya 50 waligundulika kuwa na mtoto jicho na kupewa rufaa kwaajili ya matibabu zaidi ikiwemo upasuaji ambao utafanyika Juni 13-14, 2024 katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara.

Kliniki hizi tembezi ni ushirikiano mzuri baina ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara, KCCO na Watu wa Australia katika kuwafikia wananchi waishio mbalimbali na huduma za afya.