WATAALAM WA DAWA WAWAKUMBUSHA WANAFUNZI MATUMIZI YA DAWA KWA USAHIHI
Posted on: December 21st, 2023Timu ya Wafamasia wa hospitali ya rufaa mkoa wa Manyara wakiongozwa na Bw. Sungura Meshack wametoa elimu ya matumizi ya dawa za binadamu kwa usahihi kwa Wanafunzi wa Chuo cha Manyara Institute of Health and Allied Science kilichopo wilaya ya Babati.
Akizungumza Bi. Eliachi Saria “changamoto kubwa iliyopo ni usugu wa vimelea. Tatizo ni kwamba watu wanatumia vibaya dawa kiasi kwamba vimelea vinajenga usugu kwenye dawa. Mwishowe mtu anayetumia dawa anashindwa kupata unafuu. Dawa kama ya vijiua sumu (ant-biotic) inapotumiwa vibaya ndio inajenga usugu mwilini.”
Naye Bw. Sungura Meshack alieleza kwamba “madhara yanayotokana na matumizi yasiyo sahihi ya dawa za binadamu yanaweza kupelekea kifo, kulazwa muda mrefu hospitali, ugonjwa kushindwa kutibika kwasababu ya usugu wa vimelea kuongezeka na gharama kuongezeka kutokana na kubadilishiwa dawa na kupewa dawa kubwa zaidi.
Njia za kuepuka matumizi yasiyo sahihi ya dawa unapaswa kutumia dawa za vijiua sumu (ant-biotic) pale tu unapoandikiwa na daktari, usitumie dawa ya mgonjwa mwingine ambaye anaendelea na matumizi ya dawa, usinunue vijiua sumu (ant-biotic) bila cheti cha daktari, usikatishe dozi ya dawa na tumia dozi sahihi kwa muda sahihi (kama dozi inakutaka inakutaka utumie siku saba hakikisha unazingatia siku saba).”
Wafamasia wa hospitali ya rufaa mkoa wa Manyara wamekuwa na utaratibu wa kutoa elimu ya matumizi ya dawa za binadamu kwa jamii ikiwemo Shuleni, Vyuoni na Taasisi mbalimbali ndani ya mkoa wa Manyara.