Barua Pepe | Facebook | Instagram | Twitter |

WANANCHI WAHIMIZWA KUTUMIA HUDUMA ZA KIBINGWA HOSPITALI ZA MIKOA

Posted on: October 25th, 2025

Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dkt. Seif Shekalaghe amewahimiza wananchi kutumia hospitali za Mikoa nchini kupata huduma za kibingwa, akisema Serikali imejipanga kikamilifu kuboresha huduma bora za afya katika ngazi zote.    

Dkt. Shekalaghe ametoa wito huo Oktoba 24, 2025 wakati wa ziara yake ya kikazi ya ukaguzi shirikishi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala, jijini Dar es Salaam, yenye lengo la kutathmini utoaji wa huduma kwa wananchi.

Ameeleza kuwa huduma nyingi za kibingwa zinapatikana katika hospitali za mikoa, hivyo wananchi wanapaswa kuzitumia ili kupunguza msongamano wa wagonjwa kwenye hospitali za Taifa, Kanda na Maalum.

“Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan imewekeza kwa kiwango kikubwa kwenye vifaa tiba, miundombinu, dawa na watumishi. Ukipata ajali au tatizo lolote la kibingwa, unaweza kupata tiba katika hospitali ya mkoa bila kulazimika kwenda MOI au Muhimbili. Hii itapunguza muda na gharama za matibabu kwa wananchi,” amesema Dkt. Shekalaghe.

Ameendelea kusisitiza umuhimu wa wananchi kufuata ushauri wa wataalam wa afya pamoja na matumizi sahihi ya dawa ili kuepuka usugu wa dawa.

Amebainisha pia kuwa Serikali inaendelea kuimarisha huduma za afya ngazi zote, zikiwemo hospitali za mikoa ambazo tayari zina watumishi na miundombinu ya kutosha.
Ameitaka jamii kutoa maoni yatakayosaidia kuboresha zaidi huduma katika sekta hiyo muhimu.


CHANZO - Wizara ya Afya