Barua Pepe | Facebook | Instagram | Twitter |

WANANCHI WA BABATI MJI NA VIJIJINI WAJITOKEZA KUCHANGIA DAMU

Posted on: May 22nd, 2024

Katika kuelekea Siku ya Mchangia Damu kitaifa Mkoani Manyara Juni 14 mwaka huu, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara wakishirikiana na Manyara House of Talent wameendesha zoezi la ukusanyaji damu kwa wananchi wa Kata za Gallapo, Magugu na Babati Mjini.

Ndani ya zoezi hili la ukusanyaji damu lililopewa jina la “Kwetu Festival Changia Damu Okoa Maisha” zaidi ya chupa 80 za damu zilikusanywa ambapo zitatumika kwaajili ya wagonjwa wenye uhitaji wa damu wakiwemo waliopata ajali na wamama wanaojifungua.

Sambamba na zoezi hili la ukusanyaji wa damu, Wataalam wa Afya kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara wamefanya vipimo mbalimbali vilivyoambatana na ushauri na saha kwa watu waliofika kwaajili ya kuchangia damu na burudani mbalimbali kutoka kwa Wasanii wa Mkoa wa Manyara na maeneo ya jirani

Kwa upande mwingine katika kutambua mchango wa Wadau mbalimbali waliosaidia zoezi hili, walitunukiwa vyeti vya pongezi na Afisa Utumishi Bi. Konjesta Marcel (Kwa niaba ya Uongozi wa Hospitali) kama kutambua mchango wao na ushiriki wa kampeni hizi.

Maadhimisho ya Siku ya Mchangia Damu Kitaifa yatafanyika Mkoani Manyara Juni 14 mwaka huu na yamebeba kauli mbiu isemayo “Kusherekea miaka 20 ya uchangiaji, Asante wachangia Damu.”