Barua Pepe | Facebook | Instagram | Twitter |

WAKAZI WA MJI WA BABATI WANUFAIKA NA HUDUMA YA UPIMAJI WA MACHO KATIKA KILELE CHA SIKU YA UONI DUNIANI

Posted on: October 10th, 2024

Katika kilele cha Siku ya Uoni Duniani leo tarehe 10/10/2024, Wakazi waishio Mji wa Babati wamejitokeza kupima na kupata matibabu ya macho, ambapo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara kwa kushirikiana na Shirika lisilo la Kiserikali Kilimanjaro Centre for Community Ophthalmology (KCCO) wameendesha huduma hizi katika Hospitali ya Mji wa Babati (Mrara).

Akieleza wakati wa kambi hii ya madaktari bingwa wa macho, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mrara Dkt. Giliard Francis Lupembe ameeleza kwamba faida ya kuwa na huduma hizi za macho zitapunguza shida ya uoni au kutokuona kwa wakazi waishio mji wa Babati.

Dkt. Lupembe pia ametumia fursa hii kuwapongeza Wataalam wa huduma za macho waliofika Hospitali ya Mrara kwa kuwa watawaongezea uwezo Wataalam waliopo kuendeleza huduma hii.

Kwa upande wake Meneja wa Mradi KCCO Bi. Patricia Malley ameeleza kwamba tangu kuanza kwa maadhimisho ya macho, Hospitali ya Mkoa wa Manyara na KCCO walifanya kliniki mkoba kwa kuelimisha na kufanya uchunguzi kwa wanafunzi wa shule ya msingi Sinai, Dareda na shule ya msingi Katesh B iliyopo Kata ya Katesh, Wilayani Hanang’.

Sambamba na hilo Bi. Patricia Malley ametumia fursa hii kuhimiza wakazi wa Mji wa Babati kujitokeza kufanya uchunguzi na matibabu katika Hospitali ya Mrara kwani kambi hii ni ya siku mbili tarehe 10 hadi 11 Oktoba. Pia ameongeza wanatarajia kufanya matibabu ya upasuaji siku ya Jumamosi tarehe 12/10/2024 kwa wagonjwa ambao wataonekana na matatizo yatakayo hitaji upasuaji.

Dkt. Mathias Kimaro ambaye ni mkuu wa Idara ya Macho Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara, alieleza kwamba kutokana na ushirikiano unaoendelea wa Hospitali ya Mkoa wa Manyara na Shirika la KCCO umesaidia kuwezesha huduma hizi za macho kuendelea kupatikana mkoa wa Manyara.

Maadhimisho ya Siku ya Uoni Duniani yalianza tarehe 04/10/2024 hadi 10/10/2024 na yamebeba kauli mbiu “Penda macho yako, Muhamasishe mtoto apende macho yake.”