Barua Pepe | Facebook | Instagram | Twitter |

TUONGEZE NGUVU KATIKA KUKABILIANA NA UKATILI WA KIJINSIA - KATIBU MDEMU

Posted on: September 11th, 2024

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mh. Felister Mdemu ametoa wito kwa dawati la kijinsia mkoani Manyara kuongeza nguvu na kushirikiana katika kukabiliana na ukatili wa kijinsia alipo wasili katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara leo tarehe 11/09/2024.

Mh. Felister Mdemu ametoa wito huo akiwa ziarani mkoa wa Manyara wakati akipokea taarifa fupi ya Kituo Jumuishi cha Ukatili wa Kijinsia na Ukatili Dhidi ya Watoto kilichopo hapa hospitali, taarifa iliyosomwa na Bw. Daud Donald (Mkuu wa Kitengo cha Ustawi wa Jamii).

Mh. Felister amesema kwamba taarifa zilizopo Manyara haziridhishi kutokana na matendo yanayoendelea mkoani hapa. Hivyo ni vyema kuongeza nguvu ya kukabiliana na vitendo hivi vya ukatili wa kijinsia.

Pia Mh. Felister amepongeza kwa hatua zinazoendelea kuchukuliwa na dawati la kijinsia kutokana na hali ilivyo mkoani hapa.

Kwa upande wa Timu ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii na Ofisi ya Rais-Tamisemi waliongozana na Naibu Katibu Mkuu Mh. Felister, wamesisitiza kwamba jitihada ziwepo za kupamba na hili janga la ukatili wa kijinsia wa aina yoyote. Pia wamesisitiza elimu iendelee kwa jamii ili wajue adhari za ukatili wa kijinsia hasa ukatili unapotendeka kwa watoto.

Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Manyara Bi. Wilness Kimario ambaye ni Mratibu wa Dawati la Jinsia na Watoto amesema kwamba matukio mengi mkoani hapa asilimia 60 ni ngazi ya familia na 40 nje ya familia. Hivyo iwekwe nguvu katika programu mbalimbali zinazoendelea mkoani hapa kwa kushirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali ili kufikisha elimu kwa jamii kusaidia kuweza kujilinda dhidi ya matukio ya ukatili wa kijinsia.

Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara Dkt. Katherine Magali amesema kwamba baadhi ya watu wanaofanya matukio haya ni matatizo ya saikolojia, serikali iongeze vituo vya kutoa huduma ya afya ya akili angalau kila wilaya ili kuweza kuwasaidia watu ambao wanahitaji msaada wa saikolojia.

Kulingana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), takwimu zinaonesha kuwa mkoa wa Manyara ni kati ya mikoa inayoongoza kitaifa kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia ambapo kwa takwimu Disemba 2023 kulikuwa na matukio 8,360 ambayo ni ubakaji, vipigo na ulawiti wa watoto wadogo.