RC SENDIGA AZINDUA BODI MPYA YA USHAURI YA HOSPITALI
Posted on: February 6th, 2025
Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mh. Queen Sendiga leo tarehe 6 Februari, 2025 amezindua Bodi ya Ushauri ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara, Bodi ya Wajumbe kumi (10) kati yao wawili ni Mganga Mkuu wa Mkoa wa Manyara Dkt. Andrew Method na Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara Dkt. Yesige Mutajwaa.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Bodi Mpya ya Ushauri RC. Sendiga amesema kwamba Bodi ya Ushauri ya Hospitali italeta mapinduzi na mageuzi makubwa katika Sekta ya Afya mkoa wa Manyara. Kazi ya bodi itakayoenda kufanya ni kwa maslahi ya mkoa, Wizara ya Afya na Taifa.
Pia aliongeza, bodi ina jukumu la kuhakikisha watendaji wote wa Hospitali ya mkoa wanatumia vizuri rasilimali zilizopo ambazo ni vifaa tiba na vifaa vingine kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanyika katika Hospitali.
Kwa upande mwingine RC. Sendiga alizungumzia ujio wa huduma ya usafishaji wa figo (dialysis) ambayo itaanza kutolewa hivi karibuni katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara. “Ujio wa huduma hii ina maana ya kwamba Sekta ya Afya imeendelea kuboreshwa na wananchi wa mkoa wa Manyara wamefikiwa katika huduma za afya” RC Sendiga alimalizia hivyo.