Barua Pepe | Facebook | Instagram | Twitter |

RC SENDIGA AWATEMBELEA MAJERUHI WA AJALI YA COASTER WANAOPATIWA MATIBABU HOSPITALI YA MKOA WA MANYARA

Posted on: September 1st, 2024


1 Septemba, 2024

Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mh. Queen Sendiga alifika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara kuwajulia hali majeruhi wa ajali ya Coaster ambao ni wanafunzi wa Shule ya Sekondari Endasaki iliyotokea tarehe 31.08.2024 katika eneo la Gajal, Wilayani Babati.

Akiwa hospitalini hapa RC Sendiga aliongozana na Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara Bi. Maryam Muhaji na Mratibu wa Huduma za Utabibu Mkoa Dkt. Mandala Adam siku ya jana tarehe 01.09.2024, ambapo aliwatembelea majeruhi watatu (3) wote vijana wa kike wanaoendelea na matibabu hapa hospitali.

Aidha, Mganga Mfawidhi wa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Manyara Dkt. Katherine Magali alimueleza RC Sendiga kwamba majeruhi watatu waliopo hospitalini hapa wanaendelea na matibabu na afya zao zinaendelea kuimarika.

“Jumla ya majeruhi 9 wamepewa rufaa, hospitali ya Kanda Benjamini Mkapa (2), KCMC (7). Majeruhi wengine (4) wamehamishiwa hospitali ya Mount Meru kuendelea na huduma na kuwa karibu na ndugu na jamaa. Pia majeruhi wengine 15 (wanafunzi 14 na mwalimu mmoja) waliruhusiwa kwenda nyumbani baada ya madaktari kujiridhisha kwamba afya zao zimeimarika” alieleza Mratibu wa Huduma za Utabibu Mkoa Dkt. Mandala Adam.

“Jumla ya majeruhi walioletwa hospitali ni 31, Vijana wa kike 26 na wakiume 5” aliongeza Dkt. Mandala.

RC Sendiga alitoa pongezi za dhati kwa timu ya Afya Mkoa (RHMT) na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa kwa kazi kubwa waliyofanya wakati wakitoa huduma kwa majeruhi hao.