Tahadhari dhidi ya Corona-Manyara!
Posted on: March 17th, 2020Mkoa wa Manyara umeanzisha mpango wa dharura wa kuhakikisha wananchi wanajikinga na homa inayosababishwa na virusi vya Corona, kwa kuwapatia uwezo timu ya wataalamu wa afya mkoa na wilaya ili waweze kukabiliana na mlipuko huo.
Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Manyara amesisitiza kuwa mkoa huo umejiandaa vyema kutoa elimu kwa wananchi ili kuweza kukabiliana na mlipuko wa COVID 19 ambao kwa sasa umeshawakumba watu watatu.
Amezungumza hayo Mganga mkuu wa mkoa wa Manyara Dr.Damas Kayera kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara jana Machi 18 akitoa taarifa kwa waandishi wa habari namna walivyojipanga kukabiliana na virusi vya Corona.
Amesema wanatumia njia mbalimbali kama vyombo vya habari katika kutoa elimu kwa wananchi na kwenye vituo vya kutolea huduma ya afya, namna ya kuchukua tahadhari ya kujikinga na ugonjwa unaosababishwa na virusi hivyo na ukitokea wafanye nini.
Amesema pia tayari mkoa umeshandaa vifaa pamoja na mazingira ya kutolea huduma kwa mwathirika atakaebainika kuwa na ugonjwa huo.
Alipoulizwa kuhusu upatikanaji wa vipimo vya kutambua kama mtu ameambukiwa, amesema njia inayotumika kutambua wagonjwa wa Korona ni kufanyiwa vipimo vya maabara katika Maabara Kuu ya Taifa ya Afya ya Jamii jijini Dar es Salaam.
Amewaambia wananchi wasiwe na wasi wasi kwa sababu serikali imejipanga vizuri kuweza kuwahudumia ila wazingatie kuchukua tahadhari.
Afisa afya mkoa wa Manyara Evance Simkoko amesema Kirusi cha Corona kinaenea kutoka kwa mtu mwenye maambukizi kwa njia ya kukohoa,kupiga chafya au maji maji ambayo sio rahisi kuonekana kwa macho.
Ameyataja mambo muhimu ya kuzingatia ili jamii iweze kukabiliana na kirusi hicho ni pamoja na kunawa mikono kwa sabuni kwa kutumia maji yanayotiririka kila baada ya kumaliza kufanya jambo lolote au kuingia na kutoka popote pamoja na kuepuka kugusana na mtu yeyote.
Hata hivyo mlipuko wa Ugonjwa huo haujaripotiwa kufika katika mkoa wa Manyara.