Barua Pepe | Facebook | Instagram | Twitter |

MANYARA WAZINDUA KLINIKI YA HAEMOPHILIA NA SELIMUNDU.

Posted on: November 21st, 2024

Hospitali ya mkoa wa Manyara kwa kushirikiana na hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na wadau wa afya Novo Nordisk Haemophilia Foundation (NNHF), Novemba 21,2024 wamezindua Kliniki itakayosaidia upatikanaji wa haraka na ukaribu wa huduma, vipimo na matibabu kwa wagonjwa wa Haemophilia na Selimundu.

Haemophilia ni ugonjwa usioambukiza unaotokana na damu kushindwa kuganda kutokana na kutokuwepo kabisa au upungufu wa chembechembe za protin ambazo inasababisha damu igande.

Mtu asipokuwa na hizo chembechembe akipata jeraha damu inatoka mda mrefu bila kukata hali hiyo huweza kusababisha kupoteza maisha.

Klinic hiyo ya Haemophilia na Selimundu ina vifaa mbalimbali vya kutolea huduma, mazoezi tiba kwa wagonjwa (Physiotherapy) Pamoja na vipimo maalumu vya kugundua magonjwa hayo mapema vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 17.

Hafla hiyo iliambatana na mafunzo maalum kwa wataalamu wa afya kutoka hospitali zote wilaya za mkoa wa Manyara, yenye lengo la kuboresha utoaji wa huduma kwa wagonjwa wanaosumbuliwa na magonjwa hayo yasiyo ya kuambukiza.

Akizungumza wakati wa Mafunzo hayo, Dr. John Rwegasha, Mkurugenzi wa Huduma za Tiba, Hospitali ya Taifa Muhimbili, alisema kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kuimarisha huduma za afya nchini, hasa kwa wagonjwa wa magonjwa yanayohitaji matibabu ya kipekee na kwamba Kliniki hiyo itakuwa msaada mkubwa kwa jamii ya Manyara na maeneo ya jirani.

Amesema kabla ya kuanzishwa kampeni hiyo kwa ajili ya magonjwa hayo ambayo ni ya kurithi, watoto wengi walikuwa wakipoteza maisha kwa sababu ya kufanyiwa operesheni bila tatizo kujulikana hivyo kuvuja damu nyingi na kupoteza maisha na familia kukumbana na unyanyapaa.

Huduma za vipimo na dawa kwa watakaogundulika kuwa na ugonjwa wa hamopholia na Selimundu ni Bure na kituo kitakuwa kikifunguliwa siku ya Jumanne na alhamisi kuanzia saa 2 asubuhi.