Barua Pepe | Facebook | Instagram | Twitter |

MAAZIMISHO YA KAMPENI KUPINGA UKATILI WA KIJINSIA NA UKATILI DHIDI YA WATOTO

Posted on: December 7th, 2022


Katika kampeni ya kidunia ya siku 16 kupinga ukatili wa kijinsia wenye kauli mbiu isemayo “KILA UHAI UNA THAMANI TOKOMEZA MAUAJI NA UKATILI WA KIJINSIA DHIDI YA WANAWAKE NA WATOTO” Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Manyara kupitia kitengo cha ustawi wa jamii wametoa elimu kwa jamii kupitia chombo cha habari SMILE FM RADIO.

Hadija Muwango na Daud Donald ambao ni maafisa ustawi wa jamii waliambatana na Dkt. Yusuph Mwalunu kwaajili ya kutoa elimu. Hadija Muwango alianza kwa kueleza nini maana ya ukatili wa kijinsia ambapo alieleza kwamba “ukatili wa kijinsia ni kitendo cha kumdhuru au kumuumiza mtu. Ukatili huo unaweza ukawa wa kisaikolojia, kimwili, kiuchumi na kingono.

Kwa ufupi (1)Ukatili wa kisaikolojia ni ukatili unaomfanya mtu ajihisi hana thamani Mfano: Kumtukana mtu au kumdhalilisha. Ukatili mwingine (2)Ukatili wa kimwili ni ukatili wa kumuumiza mtu Mfano: Kwa upande wa watoto kuwapiga au kuwachoma moto.

Leo tutajikita kwenye (3)Ukatili wa kingono kwasababu ndio ukatili unaofanywa kwa kiwango kikubwa na ni ukatili wenye takwimu kubwa ndani ya Mkoa wa Manyara. Tunaposema ukatili wa kingono tuna maana ya kitendo cha kumwingilia mtu kwa kumbaka au kumlawiti bila ridhaa yake, pia inaweza ikawa na maana ya kitendo chochote kinachoweza kuudhalilisha au kuutweza utu wake (Mfano: Kushikwa mwili bila ridhaa yake na mambo mengine yanayofanana na hayo). Waathirika wengi wa ukatili huu ni wanawake na watoto kwa takwimu zilizopo “Hadija alieleza”.

Hata hivyo madhara yake ni makubwa na yanaathari kubwa kwasababu sio tu yanamuathiri mtu kingono bali hata afya yake ya akili itatetereka.

Daud Donald alieleza sababu za ukatili kuendelea kushamiri. (1) Utamaduni: Hii ni kutokana na eneo husika kwa mfano ukeketaji unahusishwa sana na mambo ya kiutamaduni kwenye jamii, unaopelekea kuamini kwamba ukeketaji ni kinga dhidi ya tamaa ya kimwili. (2)Maendeleo ya sayansi na tecknolojia: Kwa kiasi kikubwa yamesababisha mmomonyoko wa maadili. (3) Migogoro ya kifamilia: Inasababisha kukosekana kwa malezi na usimamizi ulio bora kwa watoto.

Jamii inahusika kwa kiwango kikubwa katika kutokomeza huu ukatili wa kijinsia. Tunapozungumzia jamii tunazungumzia taasisi za kijamii Mfano familia, shule, kanisa na misikiti. Zote zinalojukumu la kumlinda mtoto dhidi ya ukatili. Familia ni taasisi ya kwanza katika uleaji wa mtoto, tunapoangalia malezi ya mtoto tunaangalia mtoto analelewaje, na nani anayehusika katika malezi yake. Usipompa mtoto mahitaji, kumsikiliza, kuzungumza naye, kumuelimisha mambo mbalimbali ambayo anahusiana nayo ni sawa sawa na kujivua nafasi ya mzazi au mlezi.

Kwa upande wa Dkt. Yusuph Mwalunu alipata wasaa wakuelezea huduma wanazompatia mhanga wa ukatili. Dkt. alieleza kwamba wanapopata mhanga wa ukatili kwanza kabisa watachukua vipimo ikiwemo magonjwa ya zinaa kama kaswende,VVU (Virusi vya Ukimwi),lakini pia atapimwa kama ana ujauzito (kabla ya kufanyiwa kitendo cha ukatili). Baada ya hapo tutampatia mhanga dawa za kuzuia maambukizi. Pia Dkt. alishauri kwa mhanga wa ukatili ni vyema afike hospitali mapema ndani ya masaa 72 ili apewe matibabu (dawa kinga za kuzuia maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi pamoja na ujauzito na kusisitiza mtu aliefanyiwa ukatili wa kingono “asifue nguo, asioge wala kujisaidia ili kusaidia katika ushahidi" wa kesi. Matibabu haya yote kwa wahanga wa ukatili ni bure.

Unapofanyiwa ukatili toa taarifa kwa mtu unayemwamini au vyombo husika kama mwenyekiti wa mtaa, ofisi za ustawi wa jamii na polisi. Au piga namba 116.

Afisa Ustawi walimalizia kwa kusema “Hata hivyo kitengo cha ustawi kimeendelea kutoa elimu kwenye jamii kwa kutembelea shule mbalimbali kwenye mihadhara na matukio ya kitaifa”. Hii yote ni kuwafanya wananchi wawe na uwelewa wa kuzuia na kupinga ukatili wa kijinsia.