Barua Pepe | Facebook | Instagram | Twitter |

KITUO JUMUISHI CHA MKONO KWA MKONO CHAZINDULIWA RASMI MANYARA.

Posted on: December 6th, 2024

Hatimaye kituo jumuishi cha mkono kwa mkono kimezinduliwa hii Leo mkoani Manyara katika hospitali ya rufaa ya mkoa kitakachotumika kutoa huduma za kitabibu na ushauri nasaha kwa watoto waliofanyiwa ukatili.

Akizungumza katika hafla  hiyo mgeni rasmi wa shughuli hiyo mkurugenzi wa utawala na usimamizi wa rasilimali watu Merkion Ndofi ambaye amemwakilisha katibu mkuu wa wizara ya maendeleo ya jamii jinsia wanawake na makundi maalum, ameupongeza uongozi wa mkoa pamoja na wafanyakazi wa shirika la Elizabeth Glacer Paediatric Foundation EGPAF kwa jitihada wanazofanya za kupinga ukatili kwenye jamii.

"Kipekee napenda kuwapongeza sana kwa hatua mliyochukua ya kusaidia jamii kupambana na kuzuia ukatili dhidi ya watoto, kimsingi ukatili dhidi ya watoto unapelekea mtoto kuathirika kisaikolojia, kupata madhara ya muda mfupi na ya muda mrefu."

Aidha ameongeza kuwa serikali inaendelea kushughulikia mashauri dhidi ya wanawake na watoto ikiwemo ukatili wa kimwili, kihisia, kingono na kiuchumi kipindi cha Julai 2022 hadi Juni 2024.

"Serikali kupitia jeshi la polisi imeendelea kuboresha utendaji wa madawati ya polisi ya jinsia na watoto 460 yaliyopo katika vituo mbalimbali vya polisi nchini na hadi sasa yamepokea na kushughulikia jumla ya mashauri 30,045 ya ukatili."

Akisoma taarifa ya maendeleo ya hospitali ya rufaa ya mkoa wa Manyara Mganga Mfawidhi wa hospitali Dr Yesige Mutajwaa, amesema changamoto zinazosababisha vitendo vya ukatili viongezeke ni pale ambapo kesi nyingi za ukatili zinarudishwa nyumbani na ndugu wanamalizana wao kwa wao, lakini kama hospitali licha ya changamoto hizo wameendelea kufanya jitihada kubwa za kuboresha huduma kwa waathiriwa wa ukatili ili kulinda ushahidi.

"Changamoto ya tatu ni kesi kurudishwa nyumbani kwa kutumia faini na sheria za kimila, kwa sasa tunawezesha vituo vingine vinavyotuzunguka  katika utoaji wa huduma kwa manusura wa ukatili hususani kuwahudumia waathirika pamoja na utoaji wa vifaa ili kulinda ushahidi."

Kwa upande wake Caspian Chouraya ambaye ni mkurugenzi wa EGPAF kanda ya Afrika amesema shirika hilo linafanyakazi kuhakikisha watoto hawapati maambukizi ya virusi vya UKIMWI na ukatili wa aina yeyote ile na ameishukuru serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na taasisi hiyo bega kwa bega.

"Madhumuni yetu ni kufanya kaz ili kuhakikisha watoto hawapati maambukizi ya virusi vya UKIMWI na kuwalinda dhidi ya ukatili na tunaishukuru Serikali ya Tanzania kwa kufanya kazi nasi bega kwa bega."

Mwakilishi wa USAID AFYA YANGU Anne Maphy kutoka nchini Marekani, amesema wataendelea kushirikiana na nchi ya Tanzania katika kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo kuzuia na kupinga vitendo vya ukatili.

Aidha mkuu wa wilaya ya Kiteto aliyehudhuria hafla hiyo kumwakilisha mkuu wa mkoa wa Manyara ndugu Remidius Mwema amesisitiza kuendelea kuwepo kwa mashirikiano mazuri na taasisi za dini kwani kupitia taasisi hizo itasaidia kuendelea kutoa elimu ya kupinga vitendo vya ukatili kwa wananchi.

"Tukiweza kuwaunganisha watu hawa kwenye taasisi hizi za dini itasaidia sana kupinga na kutokomeza vitendo vya ukatili kwenye jamii."

Huduma ya vituo vya mkono kwa mkono zinatolewa katika hospitali za serikali na vituo vya afya na kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kama EGPAF, imeendelea kutoa huduma katika vituo 27 vya mkono kwa mkono hapa nchini, na katika kipindi cha Julai 2022 hadi Juni 2024 nyumba 6 zimeanzishwa katika mikoa ya Arusha, Kigoma, Mara na Kilimanjaro.