Barua Pepe | Facebook | Instagram | Twitter |

KITENGO CHA AFYA YA AKILI CHAELIMISHA WANAFUNZI WA VETA MANYARA

Posted on: November 4th, 2024

Kitengo cha Afya ya Akili ambacho kipo ndani ya Idara ya Magonjwa ya Ndani kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara, kimefika leo Chuo cha Veta Manyara kuelimisha wanafunzi kuhusu afya ya akili na namna ya kupata matibabu yake.

Wakizungumza Wataalam wa Afya ya Akili walioambatana na Mkuu wa Kitengo hicho Bw. Patrick Maisson kwa nyakati tofauti tofauti wamesema kwamba, matatizo ya afya ya akili huchangiwa na mambo mbalimbali ikiwemo magonjwa ya kuridhi, matukio ambayo mtu alitendewa Mfano: Kufanyiwa ukatili wa kinjinsia ambapo humsababishia kuhifadhi tukio alilotendewa kwenye ufahamu wake na matumizi ya madawa ya kulevya ambayo huadhiri ubongo.

Wataalam waliongeza kwamba mtu akigundua anachangamoto ya afya ya akili ni vyema afike kwa Wataalam wa afya kwaajili ya kupata matibabu kwani tatizo la afya ya akili ni ugonjwa kama ugonjwa mwingine.

Kwa upande mwingine Kaimu Mkuu wa Chuo cha Veta Manyara Bi. Nansanga Massangya amempongeza Katibu wa Hospitali Bi. Vailine Oswald na Timu ya Wataalam wa Afya Hospitali ya Mkoa kufika Chuo cha Veta kwaajili ya kuelimisha tatizo la afya ya akili na kuongeza kwamba “tatizo la afya ya akili ni changamoto kwenye jamii tunazoishi hivyo wanapokuja Wataalam wa Afya wanasaidia kupunguza tatizo hili kwa Wanafunzi.”