Barua Pepe | Facebook | Instagram | Twitter |

KIKAO CHA WAKUU WA IDARA YA MACHO MANYARA NA KCCO CHA JADILI MIKAKATI YA UBORESHAJI WA HUDUMA ZA MACHO KWA MWAKA 2025/2026

Posted on: June 11th, 2025

Mkoa wa Manyara umefanya kikao muhimu Tarehe 10 Juni 2025 kilichowakutanisha wakuu wa idara ya macho kutoka ngazi ya wilaya na mkoa, pamoja na  Shirika la @kccoeyehealth Lengo kuu la kikao hicho ilikua ni kujadili na kuweka mikakati madhubuti ya kuboresha huduma za afya ya macho katika mkoa huo kwa mwaka 2025/2026.

Katika kikao hicho, washiriki walipata fursa ya kujadili changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya macho, pamoja na kuainisha fursa zilizopo kwa ajili ya kuboresha huduma hizo kwa wananchi. Miongoni mwa masuala yaliyopewa kipaumbele ni pamoja na upatikanaji wa vifaa tiba, rasilimali watu, uhamasishaji wa jamii kuhusu huduma za macho, na ushirikiano baina ya wadau wa sekta ya afya.

Kikao hiki kilifunguliwa rasmi na mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Dkt. Adam Mandala, ambaye aliwataka washiriki kutumia fursa hiyo kuweka mikakati endelevu itakayosaidia kuboresha upatikanaji na utoaji wa huduma bora za macho katika mkoa mzima.


Dkt. Mandala alipongeza Shirika la @kccoeyehealth kwa ushirikiano wao wa karibu na serikali katika kuimarisha huduma za afya ya macho, na kusisitiza kuwa mafanikio katika sekta hiyo yanahitaji mshikamano wa dhati kati ya serikali na wadau wa maendeleo.


Mbali na kupanga mikakati mipya, kikao hiki pia kilijumuisha tathmini ya mafanikio na utekelezaji wa shughuli mbalimbali za afya ya macho kwa mwaka wa fedha 2024/2025. Tathmini hiyo ililenga kutoa mwanga kuhusu hatua zilizopigwa, changamoto zilizojitokeza, na maeneo yanayohitaji uboreshaji zaidi.


Kwa pamoja, washiriki wa kikao walidhihirisha dhamira yao ya kuendeleza juhudi za kuboresha huduma za afya ya macho katika Mkoa wa Manyara, wakiahidi kuweka mikakati thabiti inayolenga kuwafikia wananchi wote, hususan wale walioko maeneo ya vijijini.