KATIBU TAWALA MANYARA AMEWATAKA WANANCHI KUPATA MATIBABU
Posted on: October 23rd, 2023Katibu Tawala Mkoa wa Manyara Bi. Karoline Mthapula amewataka mamia ya wananchi wanaofanyiwa uchunguzi wa magonjwa mbalimbali kupitia jopo la Madaktari Bingwa wanaotoa matibabu katika hospitali ya Rufaa mkoa wa Manyara kuendelea kutumia fursa ya kupima afya zao mara kwa mara pindi wanapotembelewa na madaktari bingwa.
Bi. Mthapula ametoa hamasa hiyo wakati alipokuwa akiwatembelea wananchi hospitalini hapa waliokuwa wakisubiri kufanyiwa uchuguzi wa changamoto za magonjwa mbalimbali yanayowasumbua.
Akitolea ufafanuzi Bi Mthapula amesema serikali kupitia Rais Dkt. Samia Suluhu Hassani imeamua kutumia jopo la madaktari bingwa kutembelea katika hospitali mbalimbali nchini za rufaa ili kupunguza changamoto za wananchi kusafiri kwa lengo la kutafuta matibabu na kutumia gharama kubwa hivyo akataka wananchi kutumia fursa ya kufanyiwa uchunguzi na matibabu kupitia madaktari hao.
“kipaumbele cha Dkt. Samia ni afya, afya ni kipumbele chake na ndio maana anatumia jopo la madaktari kuazisha makambi ili kuondoa changamoto za madaktari katika maeneo ambayo yamekuwa changamoto kwa wananchi wake na ndio maana sasa ameboresha miundombinu na vitendea kazi. Madaktari mnalo jukumu la kutoa huduma tena zile za kiwango cha juu”
Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa hospitali ya rufaa mkoa wa Manyara Dkt. Katherine T. Magali akitoa taarifa “tunategemea kuhudumia wagonjwa 2000 kwenye kambi hii. Tangu tumeanza kutoa huduma siku ya jana tarehe 23 Oktoba, wagonjwa wengi waliohudhuria ni katika kiliniki ya magonjwa ya ndani, wakifuatiwa na magonjwa ya pua, sikio na koo pamoja na magonjwa ya wanawake.”
Dkt. Magali alimalizia kwa kusema ndani ya kambi hii yupo daktari bingwa wa ngozi na daktari bingwa wa usingizi na ganzi kwaajili ya wagonjwa wa upasuaji.