Barua Pepe | Facebook | Instagram | Twitter |

JUMLA YA WANAFUNZI 1089 WAMEFANYIWA UCHUNGUZI WA KINYWA NA MENO

Posted on: March 19th, 2024

Katika kuhitimisha wiki ya Afya ya Kinywa na Meno leo tarehe 20 Machi jumla ya shule za msingi sita (6) na kituo kimoja (1) cha kulelea watoto yatima Wilayani Babati wamefikiwa na Wataalam wa Kinywa na Meno kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara na Hospitali ya Mji Mrara.

Wataalam wa kinywa na meno wametoa elimu kwa wanafunzi wa shule hizo ambapo walieleza “kinachosababisha meno kutoboka ni kutokuzingatia usafi wa meno mara kwa mara. Unapoacha kusafisha meno baada ya kula na matumizi ya vyakula vyenye sukari nyingi hupelekea vijidudu kuenea kwenye meno na hatimaye kutengeneza tindi kali inayosababisha kutoboka kwa meno.”

Wataalam walisisitiza kupiga mswaki mara mbili kwa siku yaani asubuhi na jioni baada ya kula ili kuondoa mabaki ya vyakula yanayosababisha vijidudu ambavyo huchangia katika uharibifu wa meno.

Jumla ya wanafunzi 1,089 wa shule za msingi Darajani, St. Clare, Bonga, Eloni, Haraa, Mutuka na kituo cha kulelea watoto yatima Hossana Home care wakiwemo wakiume na wakike wamechunguzwa kinywa na meno na kati yao wamegundulika na matatizo ikiwemo Kuoza meno, Magonjwa ya fizi, mpangilio mbaya wa meno na meno kuwa na rangi ya kahawia kutokana na kuzidi kwa madini ya floride ambapo waliogundulika na tatizo, Wataalam waliwapatia matibabu ya awali na wengine walipewa mawasiliano kwaajili ya kuwasiliana na wazazi wao kwa matibabu zaidi.