Barua Pepe | Facebook | Instagram | Twitter |

JESHI LA POLISI MKOA WA MANYARA LIMEPONGEZA UTOAJI ELIMU YA "USUGU WA DAWA (ANTIMICROBIAL RESISTANCE")

Posted on: March 28th, 2023


Timu ya wataalamu wa madawa (wafamasia) na mtaalamu wa maabara kutoka hospitali ya Rufaa mkoa wa Manyara wakiongozwa na Bi. Catherine Shirima, wametoa elimu ya usugu wa dawa na matumizi sahihi ya dawa kwa askari polisi wa mkoa huu.

USUGU WA DAWA AU UKINZANI WA VIJIUA SUMU (ANTIMICROBIAL RESISTANCE) kwa mujibu wa Shirika la Afya duniani (WHO), hutokea wakati bakteria, virusi, fangasi na vimelea vinavyobadilika kadiri muda unavyopita na hivyo kutoadhiriwa tena na dawa. Hivyo kufanya maambukizi kuwa magumu kutibu na kuongeza hatari ya kuenea kwa magonjwa makali na kifo. Kwa sababu hiyo, dawa hazifanyi kazi na maambukizo yanaendelea katika mwili, na kuongeza hatari ya kuenea kwa wengine.

Usugu wa dawa husababisha magonjwa yanayosababishwa na viemelea kuwa magumu kutibika.Ili kutibu ugonjwa unaotokana na vijidudu sugu unahitaji dawa yenye nguvu zaidi na zenye gharama na wakati mwingine hupelekea mgonjwa kulazwa hospitalini kwa uangalizi na matibabu zaidi na hivyo kuongeza gharama za matibabu na hata kusababisha kifo.“Mtaalamu wa dawa alieleza”

Pia wataalamu wa madawa waliendelea kwa kueleza, vijiua sumu (Antimicrobial) ni dawa muhimu katika kutibu magonjwa hasa yatokanayo na vijimelea vya wadudu kama bacteria, virusi, fangasi na protozoa. Ni dawa zinazotumiwa kuzuia na kutibu maambukizi kwa wanadamu, wanyama na mimea.


Dawa hizi zinapotumiwa ipasavyo huokoa maisha lakini zinapotumiwa vibaya husababisha madhara kwa mtumiaji. Mfano wa dawa za vijiuasumu ni; Ampicillin, ciprofloxacin, tetracycline, PPF, gentamycin, pen V, erythromycin na metronidazole.

MATUMIZI YASIYOSAHIHI YA  VIJIUASUMU ni

kununua dawa kiholela, kutumia dawa bila kufanyiwa uchunguzi wa daktari, kutumia vijiuasumu kutibu magonjwa yanayotokana na virusi (viral infections) mfano: mafua, kutumia dozi isiyosahihi, kutokutumia dawa kwa muda sahihi na kushindwa kumaliza dozi uliyoandikiwa.

UNAPASWA KUZINGATIA YAFUATAYO WAKATI WA KUTUMIA VIJIUASUMU

Tumia dawa pale tu unapoandikiwa na daktari, usinunue vijiuasumu bila cheti cha daktari, fanya uchunguzi wa afya kabla ya kutumia dawa, hakikisha unafahamu matumizi sahihi ya dawa ulizopewa kabla ya kurudi nyumbani kutoka kituo cha afya au duka la dawa, tumia dozi sahihi kwa muda sahihi kwa kipindi chote cha matibabu na usikatishe dozi unapojisikia nafuu. 

Kumbuka, ni muhimu kumaliza dozi ya dawa zote ulizopewa na usimpe mgonjwa mwingine dawa zako na kumbuka kutumia dawa kwa uangalifu kwa kufuata maelekezo uliyopewa na mhudumu wa afya.

Mwisho, askari polisi walitoa shurkani zao za thati kwa elimu waliyoipata huku wakihimiza elimu hii iwe endelevu.