Barua Pepe | Facebook | Instagram | Twitter |

HOSPITALI YA TAIFA YA AFYA YA AKILI - MIREMBE YAADHIMISHA SIKU YA AFYA YA AKILI DUNIANI MKOANI MANYARA

Posted on: October 10th, 2025

Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe imeadhimisha Siku ya Afya ya Akili Duniani mwaka 2025 kwa kuandaa kambi maalumu ya matibabu, ushauri nasihi na mafunzo ya afya ya akili katika Wilaya ya Babati, mkoani Manyara, ikilenga kutoa huduma bure kwa wananchi na kuelimisha watoa huduma kuhusu afya ya akili wakati wa majanga na dharura.

Maadhimisho hayo yamebeba kaulimbiu isemayo “Upatikanaji wa Huduma ya Afya ya Akili Wakati wa Majanga na Dharura,” ikilenga kuhamasisha jamii na taasisi za afya kuwekeza zaidi katika huduma za afya ya akili, hasa kwa maeneo yaliyoathirika na majanga ya asili kama vile mafuriko, maporomoko ya ardhi na matukio mengine yanayochangia athari za kihisia na kiakili kwa wananchi.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa maadhimisho hayo yaliyofanyika katika viwanja vya Motel Papaa, Babati, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe, Dk. Paul Lawala, alisema maadhimisho ya mwaka huu yamefanyika mkoani Manyara kutokana na historia ya majanga yaliyotokea hivi karibuni katika wilaya ya Hanang, ambayo yaliacha athari kubwa kwa afya ya akili ya wakazi wake.

 “Tumechagua kufanya maadhimisho haya mkoani Manyara kwa sababu mkoa huu umekumbwa na matukio kadhaa ya majanga na dharura, ikiwemo maafa ya Hanang. Athari kama hizi huacha majeraha makubwa ya kiakili, hivyo tunahakikisha jamii inapata elimu, huduma na msaada wa kitaalamu wa afya ya akili,” alisema Dk. Lawala.

Aliongeza kuwa lengo la kuweka kambi ya matibabu Babati ni kutokana na ongezeko la matukio ya ukatili wa kijinsia, ulevi uliokithiri na matumizi ya dawa za kulevya miongoni mwa wananchi wa mkoa huo, hali inayochangia ongezeko la wagonjwa wa afya ya akili wanaohitaji huduma maalumu.

“Takwimu kutoka kitengo cha tafiti na mafunzo cha hospitali yetu zinaonyesha kuwa mkoa wa Manyara unaongoza kwa idadi kubwa ya wagonjwa wa uraibu wanaopokelewa katika vituo vya afya. Kwa hiyo, ujio wetu si tu kwa ajili ya kuadhimisha, bali pia kutoa matibabu, elimu na mafunzo kwa watoa huduma,” alifafanua.

Dk. Lawala alisema timu iliyofika Manyara inajumuisha madaktari bingwa wabobezi wa afya ya akili, wanasaikolojia, wauguzi, wafamasia, wataalamu wa ustawi wa jamii na tiba kazi, ambao watakuwa Babati kwa siku tatu kutoa huduma bure za matibabu, ushauri nasihi na mafunzo kwa watoa huduma kutoka sekta mbalimbali.

“Makundi yatakayopokea mafunzo ni pamoja na watoa huduma wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara, askari polisi, na watumishi kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa. Tunataka kila mtoa huduma awe na uelewa wa namna ya kutoa msaada wa awali wa afya ya akili, hasa wakati wa majanga,” alisema.

Aidha, Dk. Lawala aliiomba Serikali kupitia Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara kuendelea kushirikiana na Hospitali ya Mirembe katika kuimarisha huduma za afya ya akili nchini.

 “Tunaomba serikali iendelee kushirikiana nasi katika kutoa elimu na mafunzo kwa jamii. Gharama kubwa za matibabu ya magonjwa ya akili zimekuwa kikwazo kikubwa kwa Watanzania wengi kupata huduma hizi. Tunashauri serikali kurasimisha kifungu maalum cha bima ya afya kwa matibabu ya akili ili Watanzania wote waweze kupata huduma hizi muhimu bila ubaguzi,” alisema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Bi. Queen Sendiga, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo, aliipongeza Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe kwa kuandaa kambi hiyo muhimu ya huduma na elimu ya afya ya akili.

Akifungua rasmi kambi hiyo ya matibabu, Mh. Sendiga alisema maadhimisho hayo yamekuja wakati muafaka, hasa baada ya mkoa huo kukumbwa na maafa ya Hanang ambayo yaliathiri kwa kiasi kikubwa afya ya kiakili ya wakazi.

“Kaulimbiu ya mwaka huu inagusisha moja kwa moja maisha yetu kama Watanzania. Baada ya maafa ya Hanang, wananchi wengi walipoteza wapendwa, makazi na mali, hali iliyoathiri afya yao ya akili. Hivyo, ujio wa Hospitali ya Mirembe ni faraja kwa wananchi wa Manyara,” alisema.

Mh. Sendiga aliongeza kuwa tatizo la afya ya akili linazidi kuongezeka kutokana na changamoto za kijamii, kiuchumi na ukatili wa kijinsia. Amesema sasa kumekuwa na ongezeko la matukio ambapo wanaume wanakuwa wahanga wa ukatili wa kijinsia kutoka kwa wenza wao, jambo linalohitaji kuangaliwa kwa umakini.

 “Zamani tulizoea kuona wanawake wakiwa wahanga wa ukatili wa kijinsia, lakini sasa hali imebadilika. Wanaume nao wameanza kuwa wahanga, na tayari kuna chama cha wanaume wanaopitia ukatili kutoka kwa wenza wao. Hii inaonyesha umuhimu wa elimu ya afya ya akili kwa jamii nzima bila kujali jinsia,” alisisitiza Mkuu wa Mkoa.

Aidha, aliahidi kuendelea kushirikiana na Hospitali ya Mirembe katika kuhakikisha huduma za afya ya akili zinaboreshwa mkoani Manyara, akisisitiza kwamba ujio huo hautabaki kuwa wa mara moja pekee.

 “Kwa niaba ya serikali, ninaahidi kuwa huu si ujio wa mwisho. Tutahakikisha watoa huduma wote wa afya mkoani Manyara wanapata mafunzo ya mara kwa mara kutoka kwa madaktari bingwa wa Hospitali ya Mirembe. Tunataka kila hospitali, kila kituo cha afya kiwe na mtaalamu anayeweza kutoa huduma ya awali ya afya ya akili,” alisema

Maadhimisho hayo yameambatana na uzinduzi wa rasmi wa kambi ya matibabu na mafunzo ya afya ya akili yatakayodumu kwa siku tatu wilayani Babati. Wananchi wametakiwa kujitokeza kwa wingi kupata huduma za matibabu, ushauri nasihi na elimu kuhusu namna ya kukabiliana na changamoto za afya ya akili bila malipo.

Vilevile, watoa huduma wa sekta za afya, ustawi wa jamii na jeshi la polisi wametakiwa kutumia fursa hiyo kujifunza mbinu za utoaji wa huduma za afya ya akili wakati wa maafa, majanga na dharura, ili kusaidia jamii kwa uharaka na kwa ufanisi zaidi.

Dk. Lawala alihitimisha kwa kusema kuwa Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe itaendelea kujikita katika kutoa elimu ya afya ya akili kwa umma, ili kuondoa unyanyapaa unaoambatana na wagonjwa wa akili na kuhakikisha Watanzania wote wanapata huduma bora, rafiki na zenye utu.

“Afya ya akili ni msingi wa maisha bora. Tunapozungumzia maendeleo ya Taifa, lazima tuweke kipaumbele katika afya ya akili ya watu wetu, kwa sababu hakuna maendeleo bila afya ya akili iliyo imara,” alisema Dk. Lawala.

Maadhimisho ya Siku ya Afya ya Akili Duniani hufanyika kila mwaka Oktoba 10 duniani kote, yakilenga kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa afya ya akili na kuchochea hatua za kitaifa na kimataifa za kuboresha huduma, sera na uelewa wa jamii kuhusu changamoto zinazohusiana na afya ya akili.

Mwaka huu, Tanzania kupitia Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe imeonyesha mfano wa kujitoa na uwajibikaji katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma, elimu na msaada wa kitaalamu bila malipo, ikisisitiza umuhimu wa kuunganisha nguvu za pamoja kati ya serikali, sekta binafsi na jamii katika kujenga taifa lenye afya bora ya mwili na akili.


Muhtasari wa Maadhimisho:

Wapi: Wilaya ya Babati, mkoani Manyara – viwanja vya Motel Papaa

Lini: Oktoba 10, 2025

Kaulimbiu: “Upatikanaji wa Huduma ya Afya ya Akili Wakati wa Majanga na Dharura”

Mratibu Mkuu: Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe

Mgeni Rasmi: Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mh. Queen Sendiga

Huduma Zitolewazo: Matibabu, ushauri nasihi, mafunzo kwa watoa huduma na elimu kwa jamii zote bila malipo.


Sent from Yahoo Mail for iPhone