ELIMU YA HOMA YA NYANI YATOLEWA KWA WATUMISHI WA AFYA
Posted on: August 21st, 2024Kutokana na ugonjwa wa homa ya nyani uliotambulika kama MPOX na kuonekana kuwa na visa vingi maeneo mbalimbali duniani ikiwemo na bara la Afrika kwenye ukanda wa Afrika Mashariki, nchi ya Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Afya imeendelea kutoa maelezo ya mwenendo wa ugonjwa huo.
Sambamba na maelezo ya mwenendo wa ugonjwa huo, hospitali ya rufaa ya mkoa wa Manyara kupitia Idara ya Magonjwa ya dharura wameelimisha watumishi wa hapa hospitali njia mbalimbali ikiwemo jinsi ugonjwa unavyosambaa, unavyoambukizwa, dalili na jinsi ya kujikinga.
“Dalili za ugonjwa huu ni homa, maumivu ya kichwa, misuli na mgongo, uchovu wa mwili, kuvimba mitoki ya mwili na vidonda vya koo. Pia unasambazwa kwa njia mbalimbali kama kula au kugusa mizoga au wanyama pori walioambukizwa mfano nyani, tumbili, sokwe au swala wa msituni. Unasambazwa pia kwa kugusana na mtu mwenye dalili za ugonjwa huu, kuugusa vitu alivyotumia mgonjwa, kugusa majimaji ya mwili na kujamiana na mtu mwenye maambukizi ya MPOX” alieleza Dkt. Juma Mabula wa Idara ya Dharura.
"Zipo njia mbalimbali ambazo mtu anapaswa kuzichukua ili kuepuka maambukizi zikiwemo epuka kugusana kwa njia ya kusalimiana, kukumbatiana, kushikana mikono na mtu mwenye maambukizi ya ugonjwa wa MPOX, unapokohoa au kupiga chafya ziba mdomo kwa kiwiko cha mkono, epuka kula au kugusa mizoga au wanyama pori wenye maambukizi ya ugonjwa huu, vaa barakoa ikiwa unaongea kwa karibu na mtu aliye na dalili za ugonjwa huu, nawa mikono kwa maji tiririka na sabuni mara kwa mara au tumia vitakasa mikono na safisha na kutakasa sehemu zote na vitu ambavyo vinaguswa mara kwa mara na watu" Dkt. Mabula aliongezea.
"Uonapo mtu mwenye dalili za ugonjwa wa homa ya nyani, toa taarifa kwenye vituo vya afya vilivyopo karibu ili kuepusha maambukizi kuenea kwa watu wengine" alimalizia hivyo.
Aidha, hospitali ya mkoa inaendelea kuelimisha umma hasa kwa mkoa wa Manyara kwa kutumia njia mbalimbali zikiwemo kuweka mabango ya elimu ya kujikinga na ugonjwa wa MPOX na njia nyingine ambazo ni rahisi kuweza kuwafikia watu wengi.
Kwa sasa hakuna mgonjwa yeyote wa MPOX nchini hivyo ni vyema kuendelea kuchukua tahadhari na kufwatilia mara kwa mara elimu kutoka kwa wataalamu wa afya sambamba na mwenendo wa ugonjwa huu.