Barua Pepe | Facebook | Instagram | Twitter |

BODI YA USHAURI YA HOSPITALI YA MKOA WA MANYARA YAVUNJWA RASMI

Posted on: January 17th, 2025

Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara imehitimisha rasmi Januari 17, 2025 muda wa uongozi wa Bodi yake ya Ushauri iliyohudumu kwa kipindi cha miaka mitatu tangu kuundwa kwake, Kikao cha kuvunja bodi hiyo kimefanyika kwa heshima kubwa na huku vyeti na Zawadi mbalimbali zikitolewa kwa wajumbe.

Mgeni rasmi katika kikao hicho alikuwa Dkt. Andrew Method, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Pia alikuwepo Mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara Shaban Gwandu, pamoja na wadau wengine wa sekta ya afya.

Akizungumza wakati wa kikao hicho, Dkt. Andrew Method ameipongeza Bodi ya Ushauri kwa mchango wake mkubwa katika kuboresha huduma za afya hospitalini hapo, na kusisitiza kuwa ushauri wa kitaalamu uliotolewa na Bodi hiyo umechangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha huduma za afya kwa wananchi wa Mkoa wa Manyara.

"Juhudi za Bodi hii zimekuwa chachu ya maendeleo makubwa tuliyoyashuhudia hospitalini hapa. Huduma za afya zimeimarika, na matokeo ya juhudi zenu yanaonekana moja kwa moja kwa wananchi wanaonufaika na huduma "Amesema Dkt. Andrew.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa, Shaban Gwandu, alieleza kuwa mafanikio ya Bodi hiyo ni mfano wa kuigwa kwani Ushauri wao umetatua changamoto mbali mbali.

Bodi hiyo ilikuwa na jumla ya wajumbe 12, chini ya uongozi wa Mwenyekiti Samuel S. Ulomi, Na imechangia mafanikio mbali mbali katika hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Manyara ikiwemo Kambi za Matibabu ya Madaktari Bingwa Bodi ilishauri kuanzishwa kwa huduma za kambi za madaktari bingwa, ambazo zimepunguza changamoto kwa wananchi waliokuwa wanalazimika kusafiri mbali au nje ya Mkoa wa Manyara kwaajili ya matibabu.

Taratibu za kuteua Bodi mpya zitaanza hivi karibuni ili kuhakikisha huduma za afya zinaendelea kuboreshwa.