Barua Pepe | Facebook | Instagram | Twitter |

WATUMISHI MANYARA RRH WAPEWA MWELEKEO WA UTOAJI HUDUMA BORA

Posted on: June 12th, 2026

Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara leo tarehe 12 Juni 2026 imefanya kikao cha watumishi wote kilicholenga kutoa taarifa mbalimbali kuhusu mwenendo wa hospitali, mafanikio yaliyopatikana pamoja na mikakati ya kuendelea kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi.

Kikao hicho kiliongozwa na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara, Dkt. Yesige Mutajwaa, akishirikiana na Afisa Utumishi, Bi. Konjesta Joseph. Katika kikao hicho, watumishi walipatiwa elimu kuhusu mapambano dhidi ya rushwa kwa kusisitiza uadilifu, uwajibikaji na kuzingatia maadili ya utumishi wa umma.

Aidha, msisitizo uliwekwa katika ujazaji sahihi wa mfumo wa PEPMIS na manufaa yake katika kuimarisha utendaji kazi, tathmini ya utendaji na utoaji wa huduma bora. Watumishi pia walikumbushwa umuhimu wa kuzingatia uvaaji nadhifu wa mavazi ya kazi ili kudumisha taswira nzuri ya hospitali na kuongeza weledi katika utoaji wa huduma.

Vilevile, kikao hicho kilitoa fursa kwa watumishi kuuliza maswali, kutoa maoni na kupata ufafanuzi kuhusu masuala mbalimbali ya kiutumishi na kiutendaji, hatua iliyochangia kuimarisha ushirikiano na mazingira bora ya kazi ndani ya hospitali.