Barua Pepe | Facebook | Instagram | Twitter |

UTEKELEZAJI WA BIMA YA AFYA KWA WOTE MKOANI MANYARA WAANZA.

Posted on: January 27th, 2026

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Sendiga,amesema kuwa, utekelezaji wa Bima ya Afya kwa wote Mkoani Manyara umeanza rasmi kwa kutoa bima za afya kwa wazee na kutoa elimu kwa wananchi mbalimbali juu ya mfuko huo kama yalivyokuwa maelekezo ya Serikali.

Aliyasema hayo wakati wa kikao chake na Waganga wakuu wa Halmashauri zote saba, Makatibu wa Afya, wakuu wa Idara zote za Mkoa pamoja na watumishi wa Afya kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Januari 27, 2026, Wilayani Babati.

"Mpaka sasa tunavyozungumza sisi tayari tumeshatoa Bima za Afya kwa wazee, wameshapata kadi zao, na wapo tayari kwa ajili ya kuanza kwenda kutibiwa, katika makundi yale muhimu ambayo ni ya awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mpango huu.Ambayo ni makundi ya wazee, watoto, wajawazito na zile kaya ambazo hazijiwezi.Sisi tumeshafanya utambuzi na tumeshatoa kadi za Bima ya Afya zipatazo saba (7),katika kadi tisa (9) ambazo tunatakiwa tutoe katika kituo cha wazee wa Magugu ambao tunafahamu hawana watu wa kuwasaidia." Alisema Mhe.Sendiga.

Aidha alisema kuwa kila kaya ya watu sita baba, mama na watoto wanne wanaweza kata Bima hii kwa gharama ya ruzuku ya shilingi 150,000 kwa mwaka mzima, na Mpango wa Mkoa ni kufikia kaya laki nne na elfu tatu ziweze kuingia kwenye mfumo huu wa Matibabu ya Bima ya Afya kwa wote lakini pia wapate elimu.

Sambamba na hayo ametoa maelekezo ya Mkoa kuwa, watendaji husika watoe elimu ya Bima ya Afya kwa umma na kuhakikisha wanazifikia kaya zote, kila Halmashauri wazifikie kaya zote,kupitia mikutano ya hadhara, kupitia redio, kwenye vikao vya kijamii, mashuleni na hata mtu kwa mtu. 

Pia amezitaka Halmashauri zisimamie uboreshaji bora wa huduma za Afya, na waongeze ubunifu wa hali ya juu kuhakikisha kwamba huduma hizi zinakua bora katika vituo vyetu vya Afya, Zahanati na kwenye hospitali zetu. Na kusema kuwa wananchi hawatakiwi kulalamika hata kero moja kwenye eneo hili, dawa zipatikane bila kisingizio kwenye vituo vya kutolea huduma.


CHANZO - Manyara RS