SHEREHE YA WAUGUZI YAFANA 2026
Posted on: May 16th, 2026Wauguzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara wameadhimisha kilele cha Siku ya Wauguzi Duniani tarehe 16 Mei 2026 kupitia shughuli mbalimbali zilizoakisi mshikamano, weledi na kujitolea katika utoaji wa huduma za afya.
Maadhimisho hayo yalitanguliwa na michezo mbalimbali iliyowakutanisha wauguzi pamoja na watumishi wa kada nyingine za afya, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha afya, ushirikiano na mahusiano kazini.
Baada ya michezo hiyo, ilifanyika hafla maalum ya kuadhimisha siku hiyo ambapo ilijikita katika kuenzi mchango wa wauguzi katika sekta ya afya. Katika hafla hiyo, wauguzi waliofanya vizuri zaidi walitunukiwa zawadi kutoka Chama cha Wauguzi Tanzania (TANNA) kama njia ya kutambua juhudi, weledi na mchango wao katika kuboresha huduma kwa wananchi.
Mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Dkt. Andrew Method, ambaye alisisitiza umuhimu wa mshikamano miongoni mwa watumishi wa afya ili kuimarisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Aidha, aliwahimiza wauguzi kuendelea kujituma katika taaluma yao na kujiunga na Chama cha TANNA ili kuimarisha maslahi na maendeleo ya kada hiyo.
Katika kuadhimisha siku hiyo, wauguzi hao pia walishiriki zoezi la uchangiaji damu lililofanyika kuanzia Tarehe 11 hadi tarehe 15 Mei 2026, hatua iliyolenga kusaidia uokoaji wa maisha ya wagonjwa wanaohitaji damu hospitalini. Sambamba na hilo, walitoa misaada mbalimbali kwa makundi yenye uhitaji, ikiwa ni sehemu ya kuonesha moyo wa huruma, upendo na kujitoa kwa jamii.



