KIHONGOSI ARIDHISHWA NA MRADI WA AFYA WA BILIONI 1.6
Posted on: June 2nd, 2026Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Mafunzo, Mh. Kenan Kihongosi, leo tarehe 02 Juni 2026, amefanya ziara katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara kwa lengo la kukagua ujenzi wa majengo ya Huduma za Dharura (EMD) na Wagonjwa Mahututi (ICU).
Katika ziara hiyo, Mheshimiwa Kihongosi amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Samia Suluhu Hassan imetoa shilingi bilioni 1.6 kwa ajili ya ujenzi wa majengo hayo, hatua inayolenga kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wananchi wa Mkoa wa Manyara na maeneo ya jirani.
"Kazi iliyofanyika hapa ni kubwa na inaonesha dhamira ya dhati ya Serikali ya Chama Cha Mapinduzi katika kuboresha huduma za afya. Miaka ya nyuma wagonjwa wengi walilazimika kusafiri kwenda KCMC au Muhimbili kupata huduma za kibingwa, lakini kwa sasa huduma nyingi muhimu zinapatikana hapa Manyara," amesema Mheshimiwa Kihongosi.
Aidha, amesema ameridhishwa na ubora wa kazi iliyofanyika pamoja na matumizi ya fedha za mradi huo baada ya kufanya ukaguzi wa kina, huku akiupongeza uongozi wa Mkoa wa Manyara na hospitali kwa usimamizi mzuri wa utekelezaji wa mradi huo.
Awali, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara, Dkt. Yesige Mutajwaa, aliwasilisha taarifa fupi ya mradi huo, akieleza kuwa ujenzi wa majengo ya Huduma za Dharura na Wagonjwa Mahututi umegharimu shilingi bilioni 1.6, umekamilika kwa asilimia 100 na tayari umeanza kutoa huduma kwa wananchi.




