Barua Pepe | Facebook | Instagram | Twitter |

IDARA YA FAMASI YATOA ELIMU GEREZA LA BABATI

Posted on: June 13th, 2026

Katika maadhimisho ya Wiki ya Famasi Kitaifa, Idara ya Famasi ya Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Manyara imepata nafasi ya kutembelea Gereza la Babati hii Leo Juni 13, 2026 kwa lengo la kutoa elimu kuhusu huduma za famasi na kuhamasisha matumizi sahihi ya dawa.

Wataalamu wa famasi walitoa elimu kwa maafisa wa gereza na wafungwa kuhusu umuhimu wa kutumia dawa kwa kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya, kuzingatia dozi zilizopangwa na kuhakikisha dawa zinatumika kwa usahihi ili kufikia matokeo yanayotarajiwa.

Aidha, washiriki walielimishwa kuhusu madhara yanayoweza kusababishwa na matumizi holela ya dawa, ikiwa ni pamoja na kutumia dawa bila ushauri wa mtaalamu wa afya, kubadilishana dawa na watu wengine na kutokamilisha dozi zilizoelekezwa.

Wataalamu hao walieleza pia nafasi ya famasi katika utoaji wa huduma za afya, wakisisitiza umuhimu wa kupata ushauri kutoka kwa mfamasia au mtaalamu wa afya kabla ya kutumia dawa yoyote. Elimu hiyo ililenga kuongeza uelewa kuhusu matumizi salama ya dawa na kuimarisha afya ya jamii kwa ujumla.

Washiriki walipata fursa ya kuuliza maswali na kupata ufafanuzi kuhusu changamoto mbalimbali zinazohusiana na matumizi ya dawa, jambo lililosaidia kuongeza maarifa na uelewa wa masuala ya afya na famasi.