Barua Pepe | Facebook | Instagram | Twitter |

'HUDUMA ZA AFYA YA KINYWA NA MENO ZIMEBORESHWA NA KUPATIKANA KARIBU ZAIDI NA WANANCHI' DC KAGANDA

Posted on: March 19th, 2026

Hayo yamesemwa leo Machi 19,2026 na Mkuu wa Wilaya ya Babati, Mhe. Emmanuela Kaganda, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Manyara, katika  Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Afya ya Kinywa na Meno Duniani yaliyofanyika kitaifa mkoani Manyara Wilayani Babati.

“Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuhakikisha huduma za afya zinaboreshwa na kuimarika. Huduma za afya ya kinywa na meno zimeboreshwa na kusogezwa karibu zaidi na wananchi”,alisema Mhe. Kaganda.

Katika Mkoa wa Manyara, halmashauri saba zimepata viti tiba vya kisasa vya kinywa na meno (dental chairs) kumi na kimoja (11), mashine nne (4) za X-ray za kinywa na meno, pamoja na mashine moja (1) ya CT scan ya kinywa, uso na taya.”

Aidha, Mhe. Kaganda aliwahimiza wananchi kujiunga na Bima ya Afya kwa Wote ili waweze kupata matibabu stahiki kwa wakati, akibainisha kuwa kifurushi hicho kinajumuisha pia huduma za afya ya kinywa na meno.

Awali,Rais wa Chama cha Wataalamu wa Afya ya Kinywa na Meno Tanzania, Dkt. Gemma Berege, alimueleza DC Kaganda kuwa katika Wiki ya Maadhimisho ya Afya ya Kinywa na Meno mkoani Manyara walitekeleza shughuli mbalimbali, zikiwemo utoaji wa elimu, uchunguzi na matibabu bure, na kufanikiwa kuwafikia wananchi zaidi ya elfu tano.

Aidha, Wataalamu wa Kinywa na meno walifika katika maeneo mbalimbali yakiwemo shule za msingi, vituo vya watoto wenye mahitaji maalumu, pamoja na Gereza la Babati.