Barua Pepe | Facebook | Instagram | Twitter |

ASKARI WAKIKE MANYARA WAFANYA MATENDO YA HURUMA KUELEKEA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI

Posted on: March 8th, 2026

Wanawake wametakiwa kusimama imara katika kutetea haki na usawa wao, kwa kuwa ni msingi muhimu wa kufikia maendeleo jumuishi ya Taifa kuelekea Dira ya Maendeleo ya mwaka 2050.

Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Mtandao wa Polisi Wanawake Mkoa wa Manyara, Mrakibu Mwandamizi wa Jeshi la Polisi, Christina Mkonongo, wakati askari polisi wanawake wa mtandao huo walipotoa msaada wa mahitaji mbalimbali kwa watoto wenye changamoto za lishe katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Manyara,ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.

Aidha, askari hao pia waliwatembelea wenzao waliokuwa wakikabiliwa na changamoto za kiafya na kuwapatia msaada ikiwa ni sehemu ya kuwafariji na kuwasaidia katika kipindi wanachopitia.

Kwa upande wake, Katibu wa Afya wa Hospitali  Aisha Elias, amewashukuru askari hao kwa msaada walioutoa kwa watoto wenye changamoto za lishe pamoja na wenzao waliokuwa wakikabiliwa na matatizo ya kiafya.

Amesema msaada huo unaonesha moyo wa kujali na mshikamano kwa jamii, huku akiomba ushirikiano huo uendelee kudumishwa.

Aidha, ametoa wito kwa wadau wengine wa maendeleo kujitokeza na kushirikiana na hospitali katika kusaidia makundi yenye uhitaji katika jamii.