WANAFUNZI WA SHULE MBALIMBALI WAENDELEA KUFIKA HOSPITALI YA MKOA KUJIFUNZA ELIMU YA AFYA
Posted on: August 24th, 2024
Siku ya leo Jumamosi tarehe 24 Agosti 2024, Walimu na Wanafunzi kutoka shule ya msingi Mutuka iliyopo Halmashauri ya Mji wa Babati, walifika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Manyara ili kupata elimu ya magonjwa ya kuambukiza pamoja na kujua huduma za afya zinazopatikana hapa hospitali.
Wageni hawa walipokelewa na Bw. Bonifasi Sangia (Muuguzi na kwa niaba ya Uongozi), Bw. Abdallah Nassor (Mkuu wa Idara ya CTC) na Bi. Magreth Mluta (Afisa Afya Mazingira) wote wa hapa hospitali ambao walieleza huduma za afya zinazopatikana na kuelimisha magonjwa mbalimbali ya kuambukiza ikiwemo kipindupindu, Virusi Vya Ukimwi na usafi wa mazingira na mtu binafsi.
Bw. Bonifasi alielimisha ugonjwa wa kipindu pindu jinsi unavyosambazwa, njia za kuepukana nao na matibabu yake ambapo alitoa msisitizo kwamba ugonjwa huu unasababishwa na kula. Mtu anapokula bila ya kunawa mikono au kutumia vyombo vyenye uchafu, hubeba wadudu ambao huingia mdomoni. Tunatakiwa kuweka mazingira yetu safi ikiwemo vyoo, vyombo vya kulia chakula pamoja na kuosha mikono na kuchemsha maji kabla ya kunywa.
Aliongeza usafi wa mikono ni muhimu, kabla na baada ya kula na baada ya kutoka chooni. Hivyo tunapoosha mikono kwa maji tiririka na sabuni tunaondoa vimelea vinavyoweza kuleta kipundupindu.
Kwa upande wa Bw. Abdallah alizungumzia ugonjwa wa UKIMWI, ambapo alisisitiza kwamba ugonjwa huu unaambukizwa kwa njia mbalimbali ikiwemo kushiriki vitu vyenye ncha na mtu mwenye maambukizi ya UKIMWI.
“Njia nyingine ya maabukizi ya Virusi Vya Ukimwi hutokea pale ambapo mtu amepewa damu ya mwenye maabukizi, inaweza kuwa damu ya mtu ilitolewa na kupewa mtu mwingine” Aliongeza Bw. Abdallah.
Bi. Magreth alisisitiza kwamba elimu hii ina manufaa kwa wanafunzi kujikinga dhidi ya magonjwa ya kuambukiza ambayo yapo kwenye jamii tunayoishi. Pia itasaidia kuwaelimisha watoto wengine waliopo shuleni na kwenye jamii na wao wachukue tahadhari mbalimbali ikiwemo kujikinga na magonjwa.
Hata hivyo Walimu wa shule hii kwa kuongozwa na Mwalimu Mkuu Bw. Ramadhani Rajabu alipongeza kwa elimu iliyotolewa na Wataalam wa hapa hospitali kwa kuelimisha kwa upana zaidi kwa walimu na wanafunzi. Aliongeza, masomo ya afya yanafundishwa shuleni lakini kwa ujio wa ziara yetu leo ni kukazia zaidi kile walichofundishwa shuleni.
Ikumbukwe kwamba hii sio mara ya kwanza hospitali ya rufaa ya mkoa wa Manyara kupokea ugeni wa wanafunzi kujifunza, tarehe 26 Mei mwaka huu shule za sekondari Kwaraa, Bagara, Nakwa, Angoni na Komoto zote za Halmashauri ya Mji wa Babati zilifika hospitalini hapa kwa lengo la kufanya usafi wa mazingira na kujifunza maswala mbalimbali ya afya.