Barua Pepe | Facebook | Instagram | Twitter |

WAKUNGA ZINGATIENI WELEDI KWENYE UTOAJI WA HUDUMA - MAJALIWA

Posted on: May 5th, 2024

Waziri Mkuu wa Tanzania Mh. Kassim Majaliwa ametoa wito kwa Wakunga na wataalamu wengine wa afya nchini kufanya kazi kwa weledi na kuongeza bidii katika kutoa huduma kwa wananchi wanaowahudumia.

Amesema kuwa kada zote za afya zinasimamiwa na miiko na maadili ya taaluma na miongozo iliyowekwa. "Hivyo basi kila mmoja ahakikishe anazingatia maelekezo mahsusi ya utendaji wa kazi."

Ameyasema hayo leo Tarehe 5 Mei, 2024 alipokuwa mgeni rasmi katika Siku ya Mkunga Duniani na Mkutano Mkuu wa Chama cha Wakunga uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.

Mheshimiwa Majaliwa amesema Chama cha Wakunga kiwe mstari wa mbele katika kukemea baadhi ya Wakunga wanaofanya kazi kinyume na maadili ya taaluma zao.

Mh. Majaliwa ameongeza kuwa Serikali ya awamu ya sita imefanya kazi kubwa katika kuboresha miundombinu na mazingira ya kutolea huduma ikiwemo kujenga majengo mapya, kufanya ukarabati wa majengo ya zamani na kujenga nyumba za watumishi karibu na vituo vya kutolea huduma ili kuhakikisha watoa huduma wanapatikana wakati wote.

"Serikali imeweka juhudi kubwa katika kununua vifaa tiba, dawa, pamoja na magari ya kusafirisha wagonjwa ili kurahisisha rufaa kati ya vituo vya kutolea huduma na wakati inapotokea dharura."

Amesema Serikali imeimarisha mfumo mzima wa rufaa kwa kushirikiana na wadau unaojulikana kama M-Mama.

Aidha, amesema maboresho hayo yamezingatia sana sehemu za kutolea huduma za mama na mtoto na kuhakikisha kuwa wodi za watoto wachanga na wale wenye matatizo (Neonatal Intensive Care Units) zinajengwa kwenye hospitali za Mikoa,Wilaya na baadhi ya vituo vya afya.

"Maboresho hayo yamechangia kuimarika kwa ubora wa huduma za Afya kwa kuwa yamegusa moja kwa moja mazingira ya kazi ya Wakunga na watendaji wengine wa sekta ya afya."


CHANZO - Wizara ya Afya