Barua Pepe | Facebook | Instagram | Twitter |

WADAU NA UONGOZI WA HOSPITALI WAMESHIRIKI KIKAO CHA PAMOJA KUJADILI MASUALA YA UKATILI WA KIJINSIA

Posted on: June 10th, 2024

Wadau mbalimbali wa Kuthibiti na Kushughulikia Vitendo vya Ukatili wa Kijinsia likiwemo Dawati la Jinsia mkoa wa Manyara lililopo Wilayani Babati pamoja na Afisa Maendeleo na Afisa Ustawi wa mkoa, Wawakilishi kutoka USAID-Afya Yangu (EGPAF) na Viongozi na Watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara wamekutana leo Juni 10, 2024 katika kikao kilichofanyika hospitalini hapa ili kujadili masuala ya Ukatili wa Kijinsia na Ukatili dhidi ya Watoto.

Akizungumza wakati wa kikao hiki Dkt. Yesige Mutajwaa ambaye ni Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara alihimiza “ni vyema kuwe na mikakati bora na dhabiti ya kushughulikia vitendo hivi vya ukatili wa kijinsia na dhidi ya watoto pale vinapobainika na kufikishwa hospitalini hapa kwenye Kitengo cha kushughulikia masuala ya ukatili, ili waathirika wa vitendo hivi wapate haki zao na huduma za matibabu bila usumbufu wowote.”

Kwa upande wa Wadau katika kikao hiki wanaoshughulikia masuala ya ukatili wa kijinsia mkoani hapa walisisitiza kwamba ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha vitendo hivi vinakemewa na kutoa ushirikiano katika kuwalinda waathirika wa ukatili.

Waliongeza kwamba matukio yatakayobainika mapema yashughulikiwe kwa wakati na katika nyanja tofauti.

Kikao hiki kilichojumuisha Wadau na Uongozi wa hospitali kina lengo la kuongeza uelewa kwa jamii juu ya uwepo wa Kituo cha Huduma Jumuishi cha kushughulikia manusura wa ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto ambapo huduma hizi stahiki zitapatikana muda wote katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara.