Barua Pepe | Facebook | Instagram | Twitter |

UHABARISHAJI JUU YA HUDUMA ZA AFYA

Posted on: September 8th, 2022

Timu ya wawakilishi kutoka hospitali ya Rufaa Mkoa wa Manyara imetembelea kambi za Sabato zilizofanyika mkoani Manyara tarehe 4-9 Septemba, 2022 kwa lengo la kuhabarisha umma juu ya Huduma za Kiafya zitolewazo na Hospitali.

Uhabarishaji huu uliambatana na ujenzi wa mahusiano mema kati ya Hospitali na wadau wa kidini. Wawakilishi walipokelewa na Mchungaji Ezra A. Juma wa Sabato na kupewa fursa ya wastani wa nusu saa ili kuweza kuhabarisha umma juu ya Huduma hizo.

Bw. Abubakari Mjaka mhamasishaji wa Huduma za Afya toka Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Manyara alianza kwa kuwashukuru viongozi wa kanisa juu ya fursa hii nzuri waliyoitoa kwa waamini wao ili wahabarike juu ya huduma za afya zinazotolewa katika hospitali ya Rufaa Mkoa wa Manyara.

Bw. Abubakari Mjaka alitaja sehemu za huduma hizo ikiwemo; huduma za madaktari bingwa, maabara, upasuaji, utengamavu (physiotherapy), kulaza wagonjwa, mionzi na picha za ndani (x-ray, utrasound, ECHO na ECG), kinywa na meno, macho na uzalishaji hewa tiba ya oksijeni kwa matumizi ya kiafya. Katika kutoa  huduma hizi hospitali imezingatia matumizi  ya mifumo ya kisasa ili kuwezesha utunzaji wa siri za wagonjwa na kutoa huduma kwa wakati, pia hospitali kupokea wagonjwa wa aina zote wakiwemo wa malipo ya papo papo na Bima za afya kwa kulingana na taratibu za Bima zao.

Bw. Abubakari Mjaka alimalizia kwa kuuhasa umma juu ya kujali afya zao na pale waonapo dalili mbali mbali za magonjwa basi wawahi hospitali au kituo cha afya kwa msaada zaidi.

MWISHO.