MKURUGENZI WA IDARA YA TIBA AFANYA ZIARA HOSPITALI YA MKOA WA MANYARA
Posted on: December 10th, 2024Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Tiba Dkt. Hamadi Nyembea kutoka Wizara ya Afya akiwa na Timu ya Wizara hiyo pamoja na Muwakilishi wa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Manyara Dkt. Mandala Adam walifanya ziara siku ya jana tarehe 10 Disemba, 2024 kukagua huduma zinazotolewa kwa Wateja wanaofika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara.
Katika ziara yake Dkt. Nyembea na Timu ya Wizara ya Afya walikagua huduma zinazotolewa kwenye Idara ya Wagonjwa wa Nje, Wagonjwa wa Ndani na mwisho walihitimisha ziara kukagua maendeleo ya miradi ya majengo ya Wagonjwa wa Dharura, Radiolojia na Jengo la Wagonjwa Mahututi.
Aidha Dkt. Nyembea katika ziara yake alipata wasaa wa kuongea na Watumishi katika kikao cha asubuhi (kikao cha Uwasilishwaji wa Taarifa) ambacho hufanyika kila Jumanne na Ijumaa kila wiki na kuongea na Timu ya Uendeshaji wa Hospitali, ambapo katika mazungumzo yake alisisitiza huduma bora kwa wateja wanaofika hapa hospitali.
Ziara hii ya Dkt. Nyembea iliambatana na Maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu ambayo kilele chake ni Disemba 10 ya kila mwaka, ambapo Wageni kutoka Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi Kanda ya Kaskazini na Wageni kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoa wa Manyara walifika hapa hospitali kuelimisha kuhusu swala la maadili na kuepukana na vitendo vya rushwa kazini.