"KUKAA MUDA MREFU, KUSIMAMA SANA NI CHANZO CHA MAUMIVU YA MGONGO"
Posted on: April 28th, 2025
Hayo yamesemwa leo tarehe 28 Aprili, 2025 na Afisa Fiziotherapia Bi. Stella Mgema na Bi. Shamsa Kizera kutoka Idara ya Utengamao katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara walipotembelea Ofisi ya TANROADS Manyara wakitoa elimu kwa Watumishi.
Bi. Stella Mgema ameeleza kwamba watu wanaopata maumivu ya mgongo wengi wao ni wanaoendesha vyombo vya moto kama magari yanayoenda safari ndefu. Huhisi mara kwa mara maumivu ya mgongo kwasababu ya kutokuwa na muda wa mapumziko kwa kunyoosha viungo vya mwili. Maumivu haya hutokana na uti wa mgongo kujikunja zaidi na wakati mwingine hupelekea mgonjwa kupatiwa matibabu zaidi kurejesha pingili katika hali ya kawaida.
Kwa upande wa Bi. Shamsa Kizera alieleza, watu wanaokaa ofisini kwa muda mrefu hukumbwa na changamoto hii. Hivyo wanashauriwa kutenga muda wa kunyoosha mwili au kutembea angalau mita chache.
Pia Mgema alishauri, katika kufanya kazi unapaswa kutokuinama sana, kutokukaa muda mrefu na kusimama muda mrefu na isizidi dakika 30 kukaa mahali pamoja. Kwa kufanya hivi hupunguza mgandamizo kwenye sahani za chini ya mgongo na kupunguza maumivu yanayoweza kujitokeza.
Aidha walikumbushia Kliniki ya jioni ambayo inatarajiwa kuanza tarehe 5 Mei 2025, kuanzia saa 9:30 Alasiri hadi saa 12:30 jioni kwa siku za kazi pekee.