Barua Pepe | Facebook | Instagram | Twitter |

KIKAO CHA KUPITIA MPANGO KAZI WA HOSPITALI, HMT NA WADAU WA AFYA

Posted on: March 27th, 2024

Timu ya Uendeshaji wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Manyara (HMT) imefanya kikao kazi kilichohudhuriwa na Wadau wa Afya Mkoani hapa ikiwemo  EGPAF- USAID Afya Yangu, KCCO, MATI Super brand LTD, PATHFINDER INTERNATIONAL, Ikizu Pharmacy na INTRACOM fertilizers LTD, Mwakilishi wa wajumbe wa Bodi ya ushauri ya hospitali Bi Coleta V. Shayo na Wajumbe wa timu ya usimamizi wa huduma ngazi ya Mkoa Leo tarehe 27 Machi,2024.

Mganga Mfawidhi Dkt. Katherine Magali aliwaeleza Wadau wa Afya Mpango Kazi wa Hospitali kwa kuwapitisha kwa ufupi katika shughuli zilizopangwa kufanyika kwa mwaka wa fedha 2024/2025 na shughuli zilizotekelezwa kwa mwaka wa fedha 2023/2024. Aidha alieleza, hospitali inahudumia wagonjwa wa nje (OPD) 45,000 na wagonjwa wa ndani (IPD) 6,000 kwa mwaka. Pia alieleza huduma mbalimbali zinazotolewa na hospitali ikiwemo huduma za kliniki mkoba na kambi za madaktari bingwa zenye lengo la kusogeza huduma kwa wananchi, huduma za upasuaji, huduma za utengemao, huduma za wanawake na uzazi, huduma za kijamii za kuwahudumia manusura wa ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto.

Dkt. Katherine Magali aliendelea kueleza kuwa katika kutekeleza shughuli hizo hospitali inakutana na baadhi ya changamoto ikiwemo upungufu wa badhii ya vifaa tiba vya kutolea huduma ikiwemo “Endoscopic machine, Portable ultrasound, Dialysis machine na Clinical chemistry analyser” na vifaa tiba vingine.

Wadau wa Afya walichangia maoni na kueleza kwamba watawezesha kliniki mkoba zenye tija na shughuli nyingine zinazohusika na afya ya mama na mtoto, na kuendelea kuwezesha wataalamu kwa ajili ya utoaji wa huduma za macho na kutoa vifaa tiba.

Kikao hiki kimekuwa na tija katika mwanzo mzuri wa kujenga uhusiano na Wadau na katika kuimarisha huduma za afya zinazotolewa na zenye tija kwa wananchi wa mkoa wa Manyara.