Barua Pepe | Facebook | Instagram | Twitter |

HUDUMA ZA AFYA ZIENDANE NA THAMANI YA UWEKEZAJI WA MHE. RAISI - DKT GRACE

Posted on: March 28th, 2023

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe ametoa wito kwa Watumishi wa Sekta ya afya Mkoa wa Manyara kushirikiana katika kutoa huduma za afya kwa wananchi ili kuendana na uwekezaji uliofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.


Dkt. Grace ametoa wito huo leo Mkoani Manyara wakati alipokuwa akizungumza na watumishi wa sekta ya afya wa Mkoa huo katika ziara yake ya kikazi ambapo amesema serikali ya awamu ya sita imeboresha sekta ya afya kwa kujenga hospitali, kununua vifaa na kuongeza watumishi. 

Amesema kuwa serikali imewekeza vya kutosha katika miundombinu ya afya na sasa ni wakati wa watumishi kutoa huduma bora zinazoendana na thamani ya uwekezaji uliofanyika.


 Dkt. Grace amewataka watumishi hao kuhakikisha wanawapatia elimu ya umuhimu wa lishe bora, chanjo kwa watoto chini ya umri wa miaka 5, matumizi ya vyoo bora na usafi wa mazingira.


Aidha ameelekeza wataalamu wa afya kuelimisha juu ya mimba za utotoni, ukatili wa kijinsia, maadili, mila  na desturi za malezi na makuzi ya watoto.


Pia amewakumbusha watumishi wa afya  kujilinda wanapotoa huduma kwa wagonjwa kwa kuvaa vifaa maalumu ili kuepukana na maambukizi ambapo ameelekeza wagonjwa wapatiwe elimu ya kujikinga na magonjwa Mfano kwa kunawa mikono kila wanapofika hospitalini.


“Tunapaswa kujali wagonjwa kwa kutumia lugha nzuri na kuwapa taarifa ikiwemo kumuelekeza mahali pa kupatiwa huduma na kuweka alama za maeneo ya huduma zitolewazo hospitalini”, amesisitiza Dkt.Grace.


Amesema maeneo ya Hospitali yanatakiwa kuwa safi wakati wote ili mgonjwa anapofika ajisikie kuwa salama wakati wote. 

Katika ziara hiyo ya kikazi Dkt. Grace amepata kukagua utaoji wa huduma hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara na kuongea na wananchi waliokuja kupatiwa huduma.


MWISHO