Barua Pepe | Facebook | Instagram | Twitter |

HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA WA MANYARA YATUNUKIWA CHETI CHA AFYA NA USAFI WA MAZINGIRA

Posted on: May 9th, 2024

Katika mashindano ya Afya na Usafi wa Mazingira kwa mwaka 2023 yaliyoshindanisha Hospitali za Rufaa za Mikoa 28 na Hospitali binafsi nchi nzima, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara ilishika nafasi ya Pili na kutunukiwa cheti cha Afya na Usafi wa Mazingira pamoja na fedha taslimu Tsh. Milioni mbili. 

Zoezi hili la ugawaji wa vyeti kwa washindi lilifanyika na Waziri wa Afya Mh. Ummy Mwalimu kwa niaba ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dkt. Phillip Isdor Mpango ambaye pia alikuwa Mgeni rasmi katika Hafla ya uzinduzi wa Kampeni ya Mtu ni Afya awamu ya pili iliyofanyika katika Viwanja vya Mailimoja Kibaha mkoani Pwani.

Akitangaza washindi wa usafi na usafi wa mazingira leo 9 Mei 2024 Kibaha, mkoani Pwani Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema Wizara ya Afya hufanya uhakiki wa vijiji ambavyo vimefikia kiwango cha juu cha usafi, zoezi ambalo linashirikisha vijiji ambavyo kaya zake zote zina vyoo, taasisi zilizopo katika Kijiji hicho na wananchi hawajisaidii ovyo katika maeneo ya wazi.    

"Mwaka huu tumeongeza kundi moja la Mshindi wa Ujumla kwa Ngazi ya Mkoa, ambapo Mkoa uliofikia kiwango cha juu cha usafi kwa kuwa na Vijiji vingi vilivyofikia kiwango cha juu cha usafi ni Iringa ambao wanapata zawadi ya gari". Amesema Waziri ummy.

Sherehe hii ni maadhimisho ya Miaka 50 ya Kampeni ya Mtu ni Afya ambapo kwa mwaka huu yalikuwa na Kauli mbiu “Afya Yangu Wajibu Wangu”.